Vikundi vya Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu wapatiwa mkopo wa thamani ya shilingi 460,000,000.00 katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza.
Hayo yamejiri leo tarehe 12, Machi,2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wawakilishi wa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu vilivyopatiwa mkopo wa asilimia 10 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe.Erick Shigongo.
Mhe.Erick Shigongo amewataka viongozi hao wa vikundi kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha,muda na kujituma kwa bidii ili kupata matokeo Chanya katika biashara zao na kuongeza kipato kwa familia.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo ameeleza na kufafanua kwamba kuna umuhimu wa wajasiriamali kuwa na kila sababu ya kuuchukia umaskini,kutafuta matatizo yaliyopo kwenye jamii na kuyatafutia ufumbuzi sambamba na kufanya kazi kwa juhudi ili waweze kufanikiwa katika shughuli wanazifanya katika vikundi vyao.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ambaye pia ni Afisa Elimu Sekondari Bw.Simbanilo Changiki ametoa wito kwa wajasiriamali hao kusimamia malengo ambayo wamejiwekea ambapo wataweza kufikia mafanikio waliyoyakusudia, sambamba na kurejesha mikopo hiyo ambayo haina riba kwa wakati ili vikundi vingine vyenye sifa viweze kukopa fedha hizo.
Katika vikundi 81 vya Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu vimeweza kunufaika na mkopo wa asilimia 10 kwa mchanguo ufuatao ambapo vikundi 47 ni vikundi vya wanawake shilingi 208,500,000.00,vikundi 30 ni vijana shilingi 231,000,000.00 na vikundi 4 ni vya watu wenye ulemavu shilingi 20,500,000.000 na kufanya jumla shilingi 460,000,000.00 ambazo zimekopeshwa.
Aidha lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kimkakati wa namna ya usimamizi na uendeshaji wa biashara wanazozifanya katika vikundi hivyo.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa