Katibu Tawala Wilaya ya Sengerema, Bw. Cuthberth Midala, amehimiza umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote kwa lengo la kutoa elimu, kupokea maoni na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu manufaa ya bima ya afya katika Halmashauri ya Buchosa.
Akizungumza leo Januari 05, 2026 katika mkutano maalum na Watendaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Midala amesema utekelezaji wa sheria hiyo unalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za afya bila vikwazo, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kujiunga na bima hiyo kwa maendeleo ya afya zao.
Katika mkutano huo, imeelezwa kuwa NHIF itaendelea kuwasajili wanachama waliokuwa wakitumia ICHF kupitia kifurushi cha huduma muhimu cha shilingi 150,000, ambapo watapatiwa namba za utambuzi za NHIF zitakazounganishwa na ICHF ili waendelee kupata huduma bila usumbufu.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Buchosa, Dkt. David Mndeba, amefafanua kuwa kuna vifurushi mbalimbali vya bima ya afya kwa mtu mmoja mmoja na kwa makundi maalum kama wachimbaji wa madini, bodaboda, wafanyabiashara na makundi mengine.
Ameeleza kuwa kaya inajumuisha watu sita baba, mama na watoto wanne na kifurushi cha jamii cha shilingi 150,000 kinahusisha huduma 372, bila kujali kaya ina mtu mmoja au sita.
Aidha, mkutano huo umejadili ulipaji wa madai kwa vituo vya kutolea huduma za afya na kusisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa usawa kwa wagonjwa wote bila ubaguzi kati ya wanaotumia bima na wanaolipa fedha taslimu.
Mkutano huo umehudhuriwa na makundi mbalimbali yakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya ushirika, mama lishe, bodaboda pamoja na wenyeviti wa zahanati na vituo vya afya.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa