Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi amewataka wananchi kuacha kutumia Uvuvi haramu wakati wa kuvua mazao ya Samaki katika Halmashauri ya Wilaya Buchosa Mkoani Mwanza.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi 21, Disemba,2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Edwin Paul Mhede wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea na kukagua mradi wa Mwalo wa Samaki na dagaa Kanyala na Ujenzi wa soko la Samaki Nyakaliro ambapo ameridhishwa na hatua za ujenzi huo.
Dkt.Mhede amefafanua na kueleza kwamba kuna tabia ya baadhi ya wananchi ya kutumia njia ambazo hazikubaliki katika kuvua mazao ya samaki,waache kufanya hivyo na badala yake watumie njia ambazo zinakubalika ili kuondokana na uvuvi haramu.
“Hili jambo tushirikiane wote tusilipinge kwa kuongea peke yake,pia tulipinge kwa vitendo na inapotokea wachache miongoni mwetu ni vizuri wakaelimishwa kuwa jambo hili si zuri na jambo hili linakemewa vikali na vyombo vyote” amesema Naibu Katibu Mkuu Dkt Mhede.
Sambamba na hilo amesisitiza kwamba kwa mtu yeyote atakayebainika anajishughulisha na uvuvi haramu atachukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo ambayo haikubaliki hata kidogo.
Aidha Naibu Katibu Mkuu amesema kwamba Serikali inatoa mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri ambapo kupitia vikundi mbalimbali wanaweza kunufaika na mikopo hiyo isiyokuwa na riba na hasa kwa watu ambao wataamua kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba.
“Moja ya eneo ambalo ni uhakika ukiwekeza pesa inarudi na ninaiona ni ufugaji wa Samaki kwa kutumia njia ya vizimba”Amesisitiza Dkt.Mhede.
Hata hivyo,kupitia Mwalo wa Kanyala Samaki aina ya sangara tani 217 na dagaa tani 774 huvuliwa kila mwaka, ambapo samaki na dagaa hutokea katika mialo ya Kanyala,Kasalazi,Gembale,Zilagula,Chembaya,Soswa na Yozu.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa