Siku ya UKIMWI duniani huadhimishwa tarehe 1 Disemba kila mwaka ili kueneza ufahamu wa ugonjwa wa UKIMWI unaosababishwa na uambukizi wa virusi vya UKIMWI.
Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yamefanyika leo tarehe 01,Disemba 2024 Kijiji cha Bugani Kata ya Bulyaheke katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa, ambapo mgeni rasmi alikuwa Diwani wa Kata ya hiyo Mhe.Ngele Nyuki Bageti ameeleza na kufafanua kwamba lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki kwenye ajenda ya udhibiti UKIMWI ambayo ni ajenda ya kidunia, kutathmini muelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI nchini na kutafakari changamoto mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya udhibiti wa Virusi vya UKIMWI(VVU).
Aidha Mhe.Bageti amesema kwamba hali ya maambukizi ya UKIMWI kwa Halmashauri ya Buchosa imepungua na kufikia asilimia 1.7 kwa mwaka 2024 ukilinganisha na mwaka 2023 ambapo kiwango cha maambukizi kilikuwa ni asilimia 2.6 hivyo Halmashauri imefanya kazi kubwa kupunguza maambukizi mapya ya ukimwi.
“Nitoe rai kwa wananchi wote wa Halmashauri ya Buchosa bila kujali rika zao waendelee kujilinda kwani kwa kufanya hivyo wataendelea kuwa na afya njema na kuendelea kufanya shughuli za maendeleo kwa ajili ya familia zao na Taifa kwa ujumla”amesisitiza Mhe.Bageti.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Bw.Florian Mkangala ameeleza kwamba katika kupambana na kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI,afua mbalimbali zimetekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ikiwa ni pamoja na Kutoa Elimu kwa wananchi,ushauri nasaha na upimaji,dawa kinga (PEP,PreP),ugawaji wa kondomu pamoja na Tohara.
Hata hivyo Halmashauri katika kutekeleza afua za VVU/UKIMWI imekua ikishirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali kama vile ICAP,ELECT-ELVD,(TB HIV),AMERICARE (PMTCT) lengo kuu ni kufikia malengo ya millennia ya 95 tatu ikifikapo 2030.
Maadhimisho hayo yameaambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo upimaji wa VVU na utoaji ushauri nasaha,utoaji wa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza, Elimu ya Lishe pamoja na Upimaji wa hiari wa VVU (Virusi vya Ukimwi).
Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kwa mwaka 2024 inasema 'Chagua njia sahihi tokomeza UKIMWI'.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa