Mkuu wa Wilaya ya Sengerema aipongeza Halmashauri ya Buchosa kwa kuvuka lengo la Ukusanya wa Mapato kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na kuwataka Madiwani kuendelea kusimamia kikamilifu ukusanya wa mapato kwa mwaka mpya wa fedha 2024/2025.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe.Senyi Ngaga ameyasema hayo jana Agosti 21, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa la kujadili taarifa za robo ya nne Aprili hadi Juni 2024, ambapo amewapongeza Waheshimiwa Madiwani na Menejimenti kwa kushirikiana pamoja katika kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Aidha Bi.Ngaga ameipongeza Halmashauri kuwa kuendelea kusimamia vizuri miradi ya Maendeleo pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo imetekelezwa kwa sehemu kubwa,hivyo ametoa rai kwamba kwa Miradi ambayo bado haijakamilika wahakikishe inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma.
Kwa upande mwingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Sengerema amewakumbusha Madiwani kuwahimiza wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 2024.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa Mhe.Idama Kibanzi ameeleza na kufafanua kwamba kama Halmashauri wamejipanga kikamilifu kwa mwaka mpya wa fedha 2024/2025 kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Sambamba na hiyo, Mhe. Kibanzi amesema kwa niaba ya Waheshimiwa Madiwani watahakikisha wanasimamia kikamilifu fedha zote za miradi ya Maendeleo kwa kila Kata ikiwemo miradi ya Afya,Elimu na Maji ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo kwa wakati.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Sengerema Bi.Waridi J.Mngumi ametoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani kwenda kuwahamisha wananchi kujitokeza kushiriki kwenye uboreshaji wa Daftari la kudumu la mpiga kura ili baadaye waweze kushiri kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Naye Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Kazunzu Mhe.Zena J.Mbiso amemshukuru Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha nyingi za mradi mkubwa wa maji Kata ya Kazunzu na maeneo mengine ya Halmashauri ya Buchosa pamoja na miradi mingine ya Afya,Elimu na Miundombinu ya barabara.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe, Senyi Ngaga akitoa maelekezo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne mwaka wa fedha 2023/2024 jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri,ambapo amewapongeza waheshimiwa Madiwani pamoja na Watumishi kwa ushirikiano katika kufanya kazi kwa pamoja.
Waheshimiwa Madiwani wakishiriki na kutoa maoni na ushauri katika kikao cha Baraza la Madiwani hapo jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri kwa robo ya nne Aprili hadi Juni 2024.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa