Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa limefanya ziara ya Kikazi,katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza yenye lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya Uendeshaji wa Halmashauri ikiwa ni pamoja na ukusanyaji Mapato.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa wakiwa wameambatana na wataalamu mbalimbali katika wa Halmashauri hiyo wamefanya ziara leo tarehe 6,Desemba,2024 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa lengo la kujifunza namna ya kuongeza mapato kupitia Miradi mbalimbali.
Akiongea wakati wa Mafunzo hayo katika ukumbi wa mikutano Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Bw. Erick Mvati ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza imebua vyanzo mbalimbali vya mapato kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha ili kutekeleza Miradi ya maendeleo pamoja na kuwashirikisha wananchi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kwa sasa jamii imejengewa uwezo juu ya uibuaji wa miradi ambayo wataweza kuitekeleza na kuikamilisha bila kutegemea usaidizi kutoka Serikalini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mhe.Idama Kibanzi amempongeza Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza pamoja na watendaji wote kwa kuweza kushirikiana vyema katika kukuza mapato ya Jiji pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi huku akiahidi kwenda kufanyia kazi yote waliyojifunza.
“Kipekee naomba kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa mapokezi mazuri kutoka kwenu na pia kujitoa kwenu kutupatia Elimu hii ya ukusanyaji wa kodi na utekelezaji wa Miradi, Hakika ziara yetu imekua yenye mafanikio makubwa kwani tumejifunza mambo mengi na mazuri na tutayafanyia kazi pindi tutakaporejea Buchosa“Amesema Mhe. Kibanzi.
Sambamba na hilo, Waheshimiwa hao Waliweza kujifunza mbinu mbalimbali za uwekezaji ambapo kwa Jiji la Mwanza wamewekeza kwenye ujenzi wa soko kuu la kisasa,Stendi kuu ya kisasa ya mabasi Nyegezi,Ujenzi wa Shule za Medium pamoja na Sekta Uvuvi ambayo ni Chachu ya kuongeza mapato kwa Jiji hilo kwani muundo wa ujenzi wa masoko hayo ni rafiki kupelekea Halmashauri kupata mapato zaidi.
Vilevile Madiwani na watalamu hao Waliweza kutembelea shamba la samaki eneo la Luchelele Kisoko kujifunza namna ufugaji wa Samaki kwa kutumia vizimba ambapo kupitia ufugaji huo mapato ya Halmashauri ya Jiji yanaongezeka.
Katika hatua nyingine Madiwani wametoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kwa kuandaa ziara ya mafunzo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia vyanzo mbalimbali na namna ya usimaiaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwenye Halmashauri hizo.
Naye mkazi wa Luchelele Bw.Fikiri Elias ambaye mnufaika wa mradi wa ufugaji Samaki kwa kutumia vizimba amesema mradi huo umemsadia kujiajiri ambapo kupitia mazao ya Samaki anapata faida na hivyo hafikiri kuajiriwa sehemu nyingine.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa