Mwenge wa Uhuru kitaifa wazindua,kukagua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Bilioni 2.9 katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava jana tarehe 06 Oktoba, 2024 amezindua,kukagua na kuweka jiwe la msingi katika miradi 6 ambayo ni Mradi wa Vyumba viwili vya madarasa Nyehunge,Mradi wa umwagiliaji Sukuma,Mradi wa Kituo cha Afya Nyakasungwa,Mradi wa upandaji miti,Mradi wa Vijana na mradi wa Maji katika Kijiji cha Kasela Kata ya Nyakaliro.
Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava amezindua mradi wa skimu ya umwagiliaji iliyojengwa kwa shilingi Bilioni 2. 4 kupitia tume ya taifa ya umwagiliaji kwenye kijiji cha Sukuma kilichopo Kata ya Bukokwa.
Akizungumza na wananchi wa Sukuma, Magurukenda na maeneo ya jirani, ndugu Mnzava ameipongeza serikali kwa kutekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo na amebainisha kuwa itawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji kwa kufanya shughuli hizo katika kipindi chote cha mwaka pasipo kusubiri mvua.
Bw.Mzanva amewaondoa hofu wananchi kwamba mradi huo sio kwa ajili ya wawekezaji na katika hilo amewahakikishia kuwa mradi huo ni kwa ajili ya wananchi na kwamba serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuwainua wananchi wake kiuchumi.
"Mradi huu ni kwa ajili ya wananchi sio wawekezaji, naomba mpuuze maneno na minong'ono inayosema kwamba mradi huo umetekelezwa kwa ajili ya wawekezaji tumieni fursa hii kuongeza uzalishaji kwenye mazao ya chakula, matunda na mbogamboga." Amesema Kiongozi wa mbio za Mwenge.
Hata hivyo Mbio za Mwenge wa uhuru umezindua madarasa 2 na matundu 6 ya vyoo katika shule ya awali na msingi Nyehunge iliyotekelezwa na serikali kwa thamani ya shilingi milioni 55.8 kupitia mradi wa GPE LANES kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye Zahanati ya Nyakasungwa ambapo Milioni 250 za mapato ya ndani yakijenga majengo ya OPD na maabara.
Katika hatua nyingine Mwenge wa Uhuru umezindua mradi wa maji kwenye kijiji cha Kasela wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni moja kwa siku wenye thamani ya Milioni 218 ambapo kiongozi wa mbio hizo amewapongeza wasimamizi (RUWASA) kwa kuongeza hali ya upatikanaji wa maji safi kutoka 10% hadi 85%.
Mbio za Mwenge zimekimbizwa kwa umbali wa kilomita 68.6 ambapo umezindua,kukagua na kuweka jiwe la msingi miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 2.9 katika Halmashauri ya Wilaya ya buchosa.
Buchosa District Council
Anuani: 44 Buchosa - SENGEREMA
Simu: 0759941297
Simu ya kiganjani: 0765029662
Barua pepe: ded@buchosadc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Hamlashauri ya Wilaya ya Buchosa. Haki zote zimehifadhiwa